Sunday, August 4, 2013

VYOMBO VYA HABARI NCHINI VYATAKIWA KUANDIKA HABARI ZA KILIMO


Na  Esther Macha wa  matukiodaima.com Mbeya
VYOMBO vya habari nchini vimetakiwa  kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha jamii kuhusiana na masuala ya kilimo kwanza kwa wakulima badala ya kukaa na kuandika mambo ambayo hayasaidii kuelimisha wakulima katika maonyesho hayo.
Kauli hiyo imetolewa jana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw. Deodatusi Kinawiro wakati wa majumuisho na waandishi habari mara baada ya kutembelea  mabanda ya maonyesho ya wakulima ya nane nane  yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale vilivyopo mjini hapa.
“Kama wanahabari mna jukumu kubwa la kupeleka taarifa kwa wananchi hasa waliopo vijijini ambao hawafahamu  jambo lolote ambalo linaendelea katika viwanja hivi vya maonyesho ,kupitia kwenu wataweza kufahamu njia mbali mbali za kilimo cha kisasa ambacho kitawafanya kuondokana na kilimo cha kizamani”alisema Bw. Kinawiro.
Hata hivyo alisema kuwa endapo waandishi wa habari watakuwa mstari wa mbele kupeleka taarifa hizo kwa wananchi kuhusiana na mambo mbali mbali ambayo yanaendelea katika maonyesho hayo kutaweza kusaidia wakulima kufahamu masuala ya kilimo .
Aidha Kaimu Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka wanahabari  kuendelea kutangaza suala la kilimo  kwa kutumia mitamndao ya kijamii  kuzungumzia kilimo cha kisasa ikiwa ni pamoja na kutumia pembejeo za kisasa.
“Ndugu zangu wanahabari andikeni masuala ya kilimo ambayo ni mazuri  kwa wakulima hapa katika maonyesho  haya kwani hapa katika uwanja huu kuna mbinu mbali mbali za kilimo bora ambazo wakulima wanaonyesha na wakulima wengine waliopo vijijini kujifunza kupitia kwao”Alisema Bw. Kinawiro.
Akizungumzia kuhusu kuwekeza kwenye maua na matunda Kaimu Mkuu huyo wa Mkoa alizitaka halmashauri zote za Wilaya Mkoani hapa  kutumia vikundi  na watu mbali mbali  kuwekeza kwenye kilimo cha maua na matunda ili kuona halmashauri hizo zinasaidia vipi vikundi hivyo.
SOURCE:Francis godwin blog

No comments:

Post a Comment